Pata taarifa kuu
UGANDA-DRC-ADAF-USALAMA

Jeshi la Uganda ladai kuua waasi 100 wa ADF nchini DRC

Jeshi la Uganda linasema operesheni yake Mashariki mwa DRC dhidi ya waasi wa ADF NALU, imesababisha mauaji ya waasi zaidi ya 100.

Gari la jeshi la Uganda likiegeshwa kwenye Mlima wa Rwenzori, karibu na eneo la Kichwamba (kusini magharibi mwa Uganda), karibu na mpaka wa DRC, Desemba 2015.
Gari la jeshi la Uganda likiegeshwa kwenye Mlima wa Rwenzori, karibu na eneo la Kichwamba (kusini magharibi mwa Uganda), karibu na mpaka wa DRC, Desemba 2015. Gaël Grilhot/RFI
Matangazo ya kibiashara

Uganda ilituma jeshi lake nchini humo baada ya waasi hao kuwawa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mwezi huu wilayani Beni.

Jeshi la UPDF limekuwa likishirikiana na jeshi la DRC, FARDC , katika operesheni hiyo.

Mapema wiki jana jeshi la Uganda lilisema lilitekeleza mashambulizi kulenga kambi za waasi mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Jeshi la Uganda lilisema kuwa baada ya kubadilishana taarifa za kiintelijensia kati yake na Serikali ya DRC walibaini mpango wa waasi wa ADF ambao hivi karibuni walishambulia kambi ya walinda amani, kuwa walikuwa wanapanga kutatiza usalama nchini Uganda.

Kwa mujibu wa umoja wa Mataifa waasi wa Uganda wa ADF ndio waliohusika na shambulizi na kuua walinda amani 14 wa Tanzania wiki mbili zilizopita.

Kundi la ADF lilianza kwa kujaribu kumpindua rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye walidai ni tishio kwa Waislamu lakini hata hivyo likajiunga na makundi mengine na kuanza kutekeleza mashambulizi mwaka 1995.

Baada ya kufurushwa na majeshi ya Uganda magharibi mwa nchi hiyo, kundi la ADF lilihamishia shughuli zake mashariki mwa nchi ya DRC.

Kundi hili pia linalaumiwa kwa shambulio dhidi ya walinda amani wa tume ya MONUSCO mwezi Octoba mwaka huu ambapo walinda amani wawili waliuawa na wengine 12 kujeruhiwa.

Kundi hili linatuhumiwa na Serikali ya DRC pamoja na tume ya umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO kwa kuhusika na mauaji ya watu zaidi ya 700 mjini Beni tangu mwezi Octoba mwaka 2014.

Wapiganaji wengi kutoka kwenye kundi hili wanadaiwa kusajiliwa kutoka nchini Tanzania, Burundi, Kenya na hata ndani ya Somalia.

Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa kundi hilo linashirikiana pia na baadhi ya wanajeshi wa Serikali ya DRC katika kutekeleza mauaji mashariki mwa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.