rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Ahmed Abba Cameroon Boko Haram

Imechapishwa • Imehaririwa

Mwanahabari wa RFI Hausa Ahmed Abba achiwa huru

media
Ahmed Abba akiondoka katika jela ya Kondengui , jijini Yaounde Desemba 22 2017 © RFI / Polycarpe Essomba

Hatimaye, Mwanahabari wa RFI Hausa, Ahmed Abba yuko huru baada ya kuwa jela kwa muda wa miezi 29.


Hatua hii inakuja baada ya Mahakama ya rufaa siku ya Alhamisi kumhukumu jela kwa kipindi cha miezi 24 , kwa kosa la kutotoa taarifa kuhusu makundi ya kigaidi, adhabu ambayo tayari alikuwa ameitumikia.

Abba alikamatwa mwaka 2015, wakati akiwahoji wapiganaji wa Boko Haram ambao ni magaidi wanaokabiliana na jeshi la Mataifa ya Afrika Magharibi, likiongozwa na Nigeria.

Mwahabari huyo raia wa Cameroon, alifunguliwa mashtaka ya ugaidi na kushirikiana na kundi hilo na Mahakama ya Kijeshi na kupewa kifungo cha miaka 10 jela, adhabu ambayo ilibadilishwa.

Kipindi hicho chote, Abba alikanusha madai hayo na kusema kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea mbele ya Mahakama hiyo.

Baada ya kuwa huru, Abba amesema amefurahi sana na kuwashukuru wale wote waliomsaidia kutoa jela hasa uongozi wa RFI.

“Nimefurahi sana. Nimefurahi sana kuwa huru kuelekea Sikukuu ya Krismasi. Nipo hotelini na Mkuu wangu wa kazi, Yves Rocle, pamoja na Mawakili wangu na mwenzangu Polycarpe Essomba,”

“Hii ni zawadi ya Krismasi. Familia ya RFI ilifanya bidii kuhakikisha kuwa niko huru. Waliniunga mkono.Mashirika yote ya kimataifa na ya Cameroon ya kutetea haki za binadamu, waliniunga sana mkono. Asanteni sana,” alisema Abba.

Mkurugenzi wa RFI Cécile Mégie, amesema amefurahishwa sana na hatua ya kuachiwa huru kwa Abba.