Pata taarifa kuu
DRC

Mtoto wa Tshisekedi ateuliwa kuongoza muungano wa Rassemblement nchini DRC

Muungano wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hatimaye umepata kiongozi wake mpya baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa muungano huo, Etienne Tshisekedi wa Mulumba aliyefariki dunia majuma kadhaa yaliyopita jijini Brussels, Ubelgiji.

Mabango ya picha za marehemu Etienne Tshisekedi, wakati watu walipokuwa wakitoa heshima jijini Brussels.
Mabango ya picha za marehemu Etienne Tshisekedi, wakati watu walipokuwa wakitoa heshima jijini Brussels. REUTERS/Francois Lenoir
Matangazo ya kibiashara

Majukwaa ya vyama 9 vinavyounda muungano wa Rassemblement, wamemchagua Felix Tshisekedi, mtoto wa Etienne Tshisekedi kuwa rais wa muungano huo na pia kumteua Pierre Lumbi kama rais wa kamati ya mazungumzo.

Uteuzi wake umekuja wakati huu bado kukiendelea kushuhudiwa mvutano kuhusu uteuzi wa jina la waziri mkuu wa mpito.

Rais wa muungano huo atakuwa na jukumu la kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano ya Desemba 31 mwaka jana, nafasi ambayo alikuwa akiishikilia marehemu Tshisekedi kabla ya kufariki dunia.

Hata hivyo vyama vitatu vya kwenye muungano huo havikukubaliana na mabadiliko mapya yaliyotangazwa, ambapo wajumbe wake waliamua kutoka kwenye mkutano uliokuwa ukiendelea kupata viongozi.

Watu wa juu kutoka kwenye muungano huo wanasema kuwa, mgawanyiko ulioshuhudiwa wakati wa mkutano huo, ulitokana na Felix kukosa uzoefu mkubwa kisiasa hali ambayo wanasiasa kadhaa wamehoji utendaji wake.

Mgawanyiko huu unatia doa harakati zilizokuwa zikifanywa na Tshisekedi mwenyewe ambaye kwa sehemu kubwa alifanikiwa kuwaunganisha wanasiasa wa upinzani, lakini hili linaloonekana sasa ni wazi litachelewesha kuanza kwa utekelezaji wenyewe wa makubaliano ya kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.