Pata taarifa kuu
DRC

Nani anachochea mauaji ya raia wilayani Beni ?

Nani anayesababisha mauaji ya raia Wilayani Beni Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ? Hili ndilo swali linalowasumbua wakaazi wa eneo hilo mwaka 2016 unapofikia mwisho.

Waasi wa FDLR Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Waasi wa FDLR Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo AFP PHOTO / Roberto SCHMIDT
Matangazo ya kibiashara

Mwisho wa wiki iliyopita wakati wa sikukuu ya Krismasi, zaidi ya watu 30 walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na waasi.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya watu 700 wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa Wilayani Beni, Jimboni la Ituri na maeneo mengine ya Jimbo la Kivu Kaskazini.

Mbali na mauaji, makaazi ya watu yameharibiwa  kwa kuchomwa moto.

Maelfu ya watu wamekuwa wakiyakimbia makwao kwa hofu ya kuvamiwa na makundi hayo ya waasi Mashariki mwa nchi hiyo.

Watalaam wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa ukweli wa kichochezi kikubwa cha mauaji haya ni utajiri wa rasilimali Mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika ya Kati na makundi mbalimbali kwa muda mrefu yameendelea kupambana kutaka kudhibiti rasilimali hiyo.

Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani MONUSCO, na serikali nchini humo, linawashtumu waasi wa ADF NALU kutoka nchini Uganda na FDLR kutoka Rwanda kuhusika na mauaji hayo ya raia.

Meya wa mji wa Beni Bwanakawa Nyonyi, akihojiwa na Shirika la Habari ya Ufaransa AFP, aliwahi kusema kuwa anaamini kuwa mauaji hayo ya raia hutekelezwa na waasi hao ambao wamechochewa kisiasa, lakini ni akina nani? Swali ambalo hadi sasa halina jibu.

Uchunguzi wa watalaam wa Umoja wa Mataifa umeonesha kuwa, mauaji mengi pia yanachochewa na makundi ya watu wanaotaka kudhibiti biashara ya mbao lakini pia suala tata la ardhi wilayani Rutshuru na Beni.

Mwaka 2016, makabiliano yaliyosababisha mauaji yameshuhudiwa kati ya makundi ya wapiganaji wa Kinande na Wahutu.

Waasi wa Kinande ambao wanajiita Mai Mai wa Mazembe wamekuwa wakidai kuwa Wahutu kutoka Rwanda ambao wanatetewa na waasi wa FDLR, wameamua kuchukua ardhi yao ilhali wao ni wageni nchini humo.

Licha ya kuwepo kwa jeshi la Kimataifa Mashariki mwa nchi hiyo, mauaji yameendelea kushuhudiwa na raia wanaendelea kuuliza, waende wapi ?

Swali lingine linalowasumbua ni, kwanini serikali na Umoja wa Mataifa wameshindwa kuyamaliza makundi haya ya waasi ?

Ni majibu ambayo wanaendelea kusubiri kuelekea mwaka mpya wa 2017.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.