Pata taarifa kuu
DRC-KABILA

Rais Kabila kuhutubia bunge la kitaifa na baraza la Seneti

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila Kabange, anajiandaa kulihutubia bunge la kitaifa na baraza la Seneti jijini Kinshasa, hotuba anayoitoa wakati huu waziri mkuu wake Matata Ponyo akiwa amejiuzulu.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila. REUTERS/Tiksa Negeri
Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya rais Kabila kwa bunge na baraza la senet, inakuja wakati huu ambapo nchi hiyo inaelekea kwenye mabadiliko ya kisiasa na kiutawala, kufuatia makubaliano ya kitaifa yaliyofikiwa kati ya Serikali na muungano wa vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia.

Makubaliano hayo ambayo yalisimamiwa na umoja wa Afrika chini ya upatanishi wa Edem Kodjo, ilikubaliwa kuwa itaundwa Serikali ya mpito ambayo itaendelea kuongozwa na rais Josephu Kabila hadi mwaka 2018 ambapo uchaguzi mkuu mpya utafanyika.

Kwenye hotuba yake rais Kabila anatarajiwa kuelezea uelekeo wa nchi yake kisiasa na hasa mara baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kitaifa miezi miwili iliyopita, baaa ya kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mmoja wa waandamanaji raia wa DRC walioandamana hivi karibuni kupinga Serikali.
Mmoja wa waandamanaji raia wa DRC walioandamana hivi karibuni kupinga Serikali. DR

Rais Kabila pia anatarajiwa kumtangaza waziri mkuu mpya kutoka vyama vya upinzani, ambaye atachukua nafasi ya Matata Ponyo, ambaye alijiuzulu Jumatatu ya wiki hii, kupisha mchakato wa kuundwa kwa Serikali ya kitaifa nchini DRC.

Mbali na kuelezea hali ya kisiasa nchini mwake, rais Kabila pia anatarajiwa kueleza maendeleo ya amani mashariki mwa nchi yake ambako wanajeshi wa Serikali wakisaidiwa na vikosi vya kulinda amani vya MONUSCO, wanakabiliana na makundi ya wapiganaji wenye silaha ambao wamekuwa wakitekeleza uasi kwenye eneo hilo.

Hata hivyo kujiuzulu kwa waziri mkuu Matata Ponyo, kumeibua mitazamo tofauti miongoni mwa wanasiasa wa Serikali na wale wa upinzani, huku baadhi yao wakiunga mkono hatua yake kwa kuwa anatimiza yaliyokubaliwa kwenye mazungumzo, huku wengine wakidai kuwa, alitakiwa kujiuzulu ili kupisha uchaguzi mkuu mpya kufanyika.

Wafuasi wa upinzani wakiwa na picha ya kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani nchini DRC, Etienne Tshisekedi, picha ya hivi karibuni.
Wafuasi wa upinzani wakiwa na picha ya kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani nchini DRC, Etienne Tshisekedi, picha ya hivi karibuni. DR

Muungano wa upinzani unaoongozwa na mwanasiasa mkongwe nchini humo, Etienne Tshisekedi wa Mulumba, unapinga makubaliano yaliyofikiwa ambapo wanasisitiza kufanyika kwa uchaguzi mkuu na rais Kabila kuondoka madarakani na sio kitu kingine.

Muungano wa upinzani pia unaungwa mkono na baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki ambao nao hawakuunga mkono makubaliano yaliyofikiwa na walitaka kufanyika kwa maridhiano ya kitaifa kabla ya kutiwa saini na kuanza kwa mchakato wa uundwaji wa Serikali ya mpito.

Haya yote yanajiri wakati huu ambapo ujumbe wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa, ukiwa umetamatisha ziara yake nchini DRC, ziara ambayo waliianza Ijumaa ya wiki iliyopita, lengo likiwa ni kukutana na wakuu wa nchi hiyo na kufanya tathmini ya kile ambacho kinajiri kwenye taifa hilo.

Miongoni mwa watu wanaotajwa kuchukua nafasi ya waziri mkuu wa DRC, ni mwanasiasa wa upinzani aliyeshiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa, Vital Kamerhe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.