Pata taarifa kuu
FGM-UNICEF

UNICEF: Wasichana na wanawake milioni 200 duniani wamekeketwa

Zaidi ya wanawake na wasichana milioni mia mbili duniani wamekeketwa huku nusu yao wakiishi nchini Misri, Ethiopia na Indonesia, hii ni kwa mujibu wa shirika la umoja wa Mataifa.

Moja ya kifaa ambacho hutumika wakati wa ukeketaji
Moja ya kifaa ambacho hutumika wakati wa ukeketaji UN
Matangazo ya kibiashara

Nchi za Somalia, Guinea na Djibouti zinaendelea kuonesha kuwa na idadi kubwa ya wasichana na wanawake waliokeketwa kidunia, lakini kiujumla karibu nchi 30 duniani vitendo hivi vimepungua, limesema shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na watoto, UNICEF.

Wakati dunia Jumamosi ya wiki hii ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kumaliza kabisa vitendo vya ukeketaji na kufikia sifuri, umoja wa Mataifa unafanya kazi kuhakikisha mila hizi zinakoma mpaka kufikia mwaka 2030, mkakati uliotengwa kwenye mpango wa maendeleo endelevu ulioidhinishwa na baraza la umoja wa Mataifa mwezi September mwaka jana.

UN

Kati ya watu milioni mia mbili waliokeketwa, milioni 44 ni wasichana walio na umri wa chini ya miaka 14 au wadogo zaidi ya hapo.

Katika nchi 30 duniani ambako vitendo hivi vinaendelea kutekelezwa, wasichana wengi wamefanyikiwa ukeketaji hata kabla ya kufika miaka mitano ya kusherekea siku yao ya kuzaliwa, imesema taarifa ya UNICEF ambayo imesema vitendo hivi ni wazi vinavunja haki za watoto.

UNICEF inasema kuwa kwenye nchi za Somalia, Guinea na Djibout, mila ya ukeketaji ni kama imekubalika nchi nzima, amesema Claudia Cappa, mwandishi wa ripoti hii.

Cappa ameongeza kuwa kuzaliwa katika nchi hizo maana yake ni kuwa una idadi ya watu 9 kati ya 10 ambao wanauwezekano mkubwa wa kukeketwa.

Ripoti hiyo ya kina imeongeza kuwa takwimu za vitendo vya ukeketaji katika nchi ya Somalia ni zaidi ya asilimi 98, huku kwa nchi ya Guinea ni aslimia 97 na nchini Djibout ni asilimia 93, kiwango ambacho dhahiri ni kikubwa.

Kwa mujibu wa ripoti hi mpya ya dunia kuhusu ukeketaji, karibu watu milioni 70 wengi ni wasichana na wanawake kuliko ilivyokadiriwa mwaka 2014, na hii kwa sehemu kubwa imetokana na takwimu mpya zilizotolewa na Indonesia na kuongezeka kwa idadi ya watu.

Hatua ziliopigwa:

Kiujumla vitendo vya ukeketaji miongoni mwa wasichana vimepungua katika nchi zaidi ya 30, kutoka asilimia 51 mwaka 1985 hadi kufikia asilimia 37 hivi leo.

Vitendo hivi vimekuwa vikipungua sana katika nchi za Liberia, Burkina Faso, Kenya na Misri ambako hatua kubwa imepigwa kupinga mila hii.

Mwandishi wa ripoti hii ameongeza kuwa, utafiti unaonesha watu wengi wanaoishi kwenye nchi zilizotajwa wanataka mila hii ipigwe marufuku, na kwamba wanahitaji kuwepo kwa juhudi za kitaifa kuhubiri madhara ya ukeketaji.

Toka mwaka 2008, zaidi ya jamii elfu 15 wameachana na mila ya ukeketaji ikiwemo jamii zaidi ya elfu 2 kwa mwaka uliopita.

Nchi tano zimepitisha sheria kali na kufanya vitendo vya ukeketaji kuwa kosa la jinai, nchi hizo ni pamoja na Kenya, Uganda, Guinea-Bissau na hivi karibuni nchi za Nigeria na Gambia ambazo zimepitisha sheria hiyo mwaka jana.

UNICEF inasema kuwa licha ya hatua zilizopigwa, mafanikiwa yanayoshuhudiwa hayaendi sambamba na ongezeko la idadi ya watu, ambapo linataka jumuiya ya kimataifa kwenda na kasi ya ongezeko la watu duniani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.