Pata taarifa kuu
JORDAN-SUDAN-HAKI

Wasudan 800 wanaotafuta hifadhi Jordan warejeshwa nyumbani

Jumatano hii, serikali ya Jordan imewarejesha nyumbani raia 800 wa Sudan waliokua wakitafuta hifadhi. Raia hao wamekua wakidai hadhi ya ukimbizi nchini Jordan.

Wakimbizi wa Sudan mbele ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi katika mji wa Amman, Desemba 12, 2015.
Wakimbizi wa Sudan mbele ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi katika mji wa Amman, Desemba 12, 2015. AFP/AFP/
Matangazo ya kibiashara

"Watu 800 kutoka Sudan wamerejeshwa nyumbani Jumatano hii", msemaji wa serikali na Waziri wa Habari Mohamed Momani, ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.

Momani ameeleza kuwa "uamuzi wa kuwarejesha makwao raia hao wa Sudan umechukuliwa baada ya wao (raia wa Sudan) kuomba hadhi ya ukimbizi nchini Jordan."

Kulingana na kiongozi huyo, "hadhi hii haiwezi kutumika kwa kesi yao, kwa vile walikuja Jordan kwa ajili ya matibabu". "Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi (UNHCR) katika mji wa Amman haliwachulii raia hao kama wakimbizi", Momani ameongeza.

Raia kadhaa kutoka Sudan wamekua wakiandamana kwa siku kadhaa katika mahema mbele ya ofisi ya UNHCR katika eneo la Khalda, magharibi mwa mji mkuu wa Jordan.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Jordan, Idara za usalama zimevunja maandamano hayo Jumatano hii asubuhi na raia hao wa Sudan walipelekwa moja kwa moja kwenye uwanja wa ndege wa Amman.

"Jordan haina msamaha kwa kuwafukuza watu wanaotafuta hifadhi ambao wanaishi katika mazingira magumu", amejibu katika taarifa yake Joe Stork, naibu mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW).

"Jordan haipaswi kuwaadhibu raia wa Sudan kwa sababu tu walikuwa wakipinga ili waweze kupata hali nzuri ya maisha (...)", Joe Stork ameongeza.

UNHCR inakadiria idadi ya Wasudan 3500 wanaotafuta hifadhi nchini Jordan, ambao wengi walikuja kutoka mkoa wa Darfur (magharibi).

Mkoa huu umekumbwa na vita tangu mwaka 2003 kati ya waasi na majeshi ya serikali ya Rais Omar al-Bashir, na vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000.

Jordan tayari imepokea zaidi ya wakimbizi 600,000 wa Syria kwa mujibu wa UNHCR. Utawala, hata hivyo, unasema kuwa idadi idadi ya wakimbizi wa Syria nchini Jordan ni milioni 1.4, sawa na 20% ya wakazi wa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.