Pata taarifa kuu
KENYA-VATICAN-AMANI-MARIDHIANO

Papa Francis awataka viongozi wa Kenya kuwa waadilifu

Papa Francis, aliyewasili Jumatano hii nchini Kenya, nchi ambayo inakabiliwa na rushwa, ameonya dhidi ya "kukata tamaa" "kuchanganyikiwa" na "umaskini" unaotokana na ugaidi na vurugu, huku akiwatolea wito viongozi wa Kenya kufanya kazi na "uadilifu" na kwa "maslahi ya umma".

Papa Francis aangua kicheko akiambatana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kushoto) mjini Nairobi,Novemba 25, 2015.
Papa Francis aangua kicheko akiambatana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (kushoto) mjini Nairobi,Novemba 25, 2015. REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Papa Francis amewasili Jumatano hii nchini Kenya, hatua ya kwanza ya ziara yake ya siku tano barani Afrika ambayo pia itampeleka Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Papa Francis ataadhimisha Misa katika Chuo Kikuu cha Nairobi Alhamisi hii, ambapo siku hiyo imetangazwa kuwa likizo ya kitaifa. Askari polisi elfu kumi wamewekwa katika maeneo mbalimbali kwa usalama wa Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.

Katika hotuba aliyoitoa mara baada tu ya kuwasili kwake kwenye Ikulu, makazi rasmi ya Rais Uhuru Kenyatta, Papa amewataka viongozi wa dunia kulinda mazingira na kutetea maendeleo endelevu kwa kufikiria vizazi vijavyo. Papa Francis amepanda mti katika bustani ya makazi ya rais.

Papa Francis pia atazungumzia suala la tabia nchi Alhamisi wiki hii katika hotuba yake kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.

Katika hotuba yake Ikulu, Papa Francis amewatolea wito "wanaume na wanawake wote wenye nia nzuri njema kujihusisha na masuala ya maridhiano, amani na msamaha" dhidi ya "mgawanyiko wa kikabila, kidini na kiuchumi."

"Kipaumbele kwa sasa ni mazungumzo kati ya imani tofauti", amesema kwa upande wake, Rais Kenyatta, Mkatoliki kama 30% ya wananchi wake.

Kenya na Uganda zilikumbwa katika miaka ya hivi karibunina mashambulizi ya makundi ya kiislamu, na nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, kumeendelea kushuhudiwa vita kati ya Wakristo na Waislamu.

"Nakwenda kwa furaha nchini Kenya, Uganda na kwa ndugu zetu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Nina imani kuwa safari hii itazaa matunda, ya kiroho na kimwili", amesema Papa katika ndege iliyokua ikimsafirisha kwenda Kenya.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.