Pata taarifa kuu
BURUNDI-BUNGE-SIASA-USALAMA

Burundi: Agathon Rwasa ashiriki kikao cha kwanza cha Bunge

Mpinzani mkuu nchini Burundi Agathon Rwasa, ambaye alilaani na kulalamika siku tatu zilizopita kuwa mchakato wa uchaguzi ulikua kama “ mchezo wa kuigiza ” na kupinga matokeo ya uchaguzi, hatimaye ameshiriki kikao cha kwanza cha Bunge Jumatatu Julai 27 mjini Bujumbura.

Baada ya kupinga mchakato wa uchaguzi alioutaja kuwa "mchezo wa kuigiza", mpinzani kuu wa Pierre Nkurunziza, Agathon Rwasa, ameamua kushiriki kikao cha kwanza cha Bunge nchini Burundi, Jumatatu Julai 27 mwaka 2015.
Baada ya kupinga mchakato wa uchaguzi alioutaja kuwa "mchezo wa kuigiza", mpinzani kuu wa Pierre Nkurunziza, Agathon Rwasa, ameamua kushiriki kikao cha kwanza cha Bunge nchini Burundi, Jumatatu Julai 27 mwaka 2015. AFP PHOTO / PHIL MOORE
Matangazo ya kibiashara

Tume Huru ya Uchaguzi (Céni) ilitangaza kuwa muungano wa wagombea binafsi Amizero y'abarundi unaoongozwa na Agathon Rwasa ulichukua nafasi ya pili kwa kupata viti vya wabunge 30 katika uchaguzi wa wabunge na madiwani, licha ya muhusika mwenyewe kutangaza kuwa hatambui matokeo hayo kutokana na kile alichokitaja kuwa alijiondoa katika uchaguzi huo. Kushiriki kwa Agathon Rwasa bungeni ni pigo kubwa kwa upande wa upinzani.

Jioni ya Jumatatu wiki hii, upinzani nchini Burundi ulikua katika masikitiko makubwa kufuatia kitendo hiki cha Agathon Rwasa kushiriki katika kikako cha Bunge, wakati ambapo serikali kwa upande wake ikikaribisha kiktendo hicha cha Agathon Rwasa. Hata hivyo baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamekua wakisema kuwa hawana imani na Agathon Rwasa kwa kauli zake kwani kila mara maneno yake hayaambatani na vitendo, huku wengine wakitaja kuwa ni mwepesi wa kushawishika.

Kwa upande wa kambi ya Agathon Rwasa wamebaini kwamba kushiriki katika vikao vya Bunge haimaanishi kuwa wanakubaliana na matokeo ya ucaguzi, bali ni mbinu mpya wanayotumia kwa kuzuia ili Nkurunziza asifaulu kuunda serikali, kwani iwapo wataachia nafasi hiyo bungeni kura za muungano wa wagombea binafsi Amizero y'abarundi zingelipewa chama cha Uprona ambacho ni mshirika wa karibu wa chama cha Cndd-Fdd, na hivyo kuunda serikali bila hofu yoyote.

Hata hivyo baadhi ya wafuasi wa Agathon Rwasa wameelezea masikitiko yao kuona kiongozi wao anakubali kushirikiana na chama cha Cndd-Fdd ambacho kilivunja hadhari Katiba ya nchi na Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha, wakibaini kwamba Agathon Rwasa amewasaliti. Baadhi waghadhibishwa na kitendo hicho na kufikia hata kusema kuwa huenda Agathon Rwasa amekubali kushirikiana na chama cha rais Nkurunziza baada ya kupewa mamilioni ya pesa.

Hayo yanajiri wakati upande mwengine wa muungano huo wameshangazwa na kitendo hicho cha Agathon Rwasa. Baadhi ya wajumbe wa muungano huo ambao walichaguliwa kuwa wabunge walikataa kushiriki kikao cha kwanza cha Bunge cha Jumatatu wiki hii. Huenda ali hii ikazua mpasuko katika muungano huo wa wagombea binafsi Amizero y'abarundi. Lakini Charles Nditije kiongozi wa tawi la Uprona linaliounda muungano huo amesema hali hiyo haiwezi ikazua mpasuko, huku akibaini kutoelewa kwa nini Agathon Rwasa amekubali kushiriki kikao cha Bunge.

Wakati huo huo Jumuiya ya kimataifa imeendelea kupinga matokeo ya uchaguzi, huku ikiomba serikali na upinzani kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa kutafutia suluhu mgogoro unaoendelea kushuhudiwa nchi Burundi.

Vyama vingine vikuu ya upinzani vimeendelea na msimamo wao wa kupinga muhula wa tatu na kusema kutotambua matokeo ya uchaguzi kwani, rais Pierre Nkurunziza amevunja Katiba ya nchi na Mkataba wa amanai na maridhiano wa Arusha. Wengi wanahofia kuwa huenda hali hii ikazua vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na jinsi hali inavyoendelea. Mwishoni mwa juma lililopita kulitokea mapigano kati ya kundi la watu wenye silaha na wanajeshi wa Burundi katika msitu wa Rukambasi mkoani Makamba kusini mwa Burundi. Mpaka sasa haijajulikana hasara ya mapigano hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.