rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Burundi Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki Pierre Nkurunziza Umoja wa Mataifa UN

Imechapishwa • Imehaririwa

Mkutano wa marais wa (EAC) kuhusu mgogoro wa Burundi

media
hali ya sintofahamu yaendelea kushuhudiwa Burundi, ambapo polisi imekua ikinyooshewa kidole kuhusika na mauaji ya raia wasiyokua na hatia. REUTERS/Goran Tomasevic

Marais wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki wanatazamiwa kukutana Jumatatu Julai 6 jijini Dar es salaam, nchini tanzania kuhusu mgogoro unaoendelea nchini Burundi, afisa mmoja mwandamizi wa jumuiya hiyo ameiambia RFI.


Mkutano huu ulitangazwa na rais wa tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni mwenyekiti wajumuiya ya Afrika Mashariki, katika mkutano wa Umoja wa Afrika uliyofanyika hivi karibuni jijini Pritoria, nchini Afrika Kusini.

Hayo yanajiri wakati hali ya usalama imeendelea kudorora nchini Burundi, hususan katika baadhi ya maeneo ya mji wa Bujumbura. Milio ya risasi imekua ikisikika kila siku usiku katika wilaya ambazo ni kitovu cha vuguvugu la maandamano ikiwa ni pamoja na Cibitoke, Buterere, Nyakabiga, Musaga, Kanyosha na Ngagara.

Hivi karibuni viongozi wa kuu katika utawala wa Nkurunziza waliitoroka nchi na kukimbilia ugenini. Makamu wa pili wa rais Gervais Rufyikiri pamoja na spika wa Bunge Pie Ntavyohanyuma walikimbilia nchini Ubelgiji, wakibaini kwamba Pierre Nkurunziza ana lengo la kuitumbukiza Burundi katika dimbwi la machafuko.

Mshauri mkuu wa masula ya mawasiliano katika Ikulu ya rais, Willy Nyamitwe, alibaini kwamba viongozi hao hawakuitoroka nchi bali walirejea nchini mwao Ubelgiji.

Itafahamika kwamba Pie Ntavyohanyuma na Gervais Rufyikiri waliitoroka nchi hiyo baada ya kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali katika utawala wa Nkurunziza tangu chama cha Cndd-Fdd kichukuwe hatamu ya uongozi wa nchi mwaka 2005, baada ya kusitisha mapigano na kutia saini na serikali  iliyokuwepo wakati huo kwenye Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha.

Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Umoja wa Afrika walimsihi rais Nkurunziza kuahirisha uchaguzi kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu, lakini rais huyo alipuuzia mbali pendekezo hilo.

Jumatatu wiki hii uchaguzi wa wabunge na madiwani ulifanyika bila hata hivyo kuitikiwa na vyama vikuu vya upinzani.

Katika hotuba yake Jumatano Julai 1 wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru wa Burundi, rais Pierre Nkurunziza aliyaonya mataifa ya magharibi kotoingilia masuala ya ndani ya Burundi, akisema kwamba Burundi iko huru, na inapaswa kujiamulia masuala yake peke yake bila kuingiliwa na nchi za kigeni.

Wadadisi wanasema utawala wa Nkurunziza unaelekea pa baya kutokana na kuwa rais huyo amekua akidharau mapendekezo ya taasisi za kimataifa na nchi jirani.