Pata taarifa kuu
SUDAN-DARFUR

Umoja wa Mataifa waongeza muda zaidi kwa vikosi vya UNAMID kwenye jimbo la Darfur

Nchi za Uingereza na Marekani juma hili zimesema kuwa ni mapema sana kwa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani walioko nchini Sudan kwenye jimbo la Darfur kuondolewa wakati huu baraza la usalama likiongeza muda wa mwaka mmoja zaidi kwa vikosi hivyo.

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura.
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura. UN Photo/Loey Felipe
Matangazo ya kibiashara

Haya yanajiri wakati huu Umoja huo ukijadili mpango wa namna ya kuanza kuviondoa vikosi hivyo vya UNAMID ambavyo vina wanajeshi elfu 17 vinavyosimamiwa na Umoja wa Afrika.

Licha ya mjadala huu, nchi wanachama 15 za baraza la usalama zimekubaliana kimsingi na kuweka wazi kuwa ni lazima Serikali ya Khartoum ihakikishe inaonesha nia ya dhati katika kutatua mzozo wa Darfur kabla ya kuondolewa kwa wanajeshi wa kulinda amani.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, balozi wa Uingereza Matthew Rycroft amesema kwa wakati huu kuzungumzia suala la kuwaondoa wanajeshi wa kulinda amani kwenye jimbo la Darfur ni mapema sana kwakuwa bado hali ni tete kwenye eneo hilo.

Hivi karibuni kumeshuhudiwa makabiliano makali kwenye jimbo la Darfur wakati huu jeshi la Sudan likizidisha mashambulizi dhidi ya ngome za waasi, ambapo mpaka sasa watu zaidi ya elfu 78 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Kwa upande wake, balozi wa Marekani kwenye Umoja huo, Samantha Power, amesema kuwa kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama kwenye eneo la Darfur na pia kutokana na wananchi wengi kukimbia makazi yao, uwepo wa vikosi vya kulinda amani ni muhimu hasa katika wakati huu.

Katika azimio lililopitishwa jana jioni na nchi wanachama wa baraza la usalama, linaeleza kwa kina namna bora ya kupata suluhu ya kisiasa kwenye eneo hilo, mpango wa kuwalinda raia, kuruhusu mashirika ya misaada pamoja na kueleza kwa kina chanzo cha mzozo unaoendelea.

Kwenye kikako hicho wajumbe walikubaliana kuongeza muda wa mwaka mmoja zaidi kwa vikosi vya UNAMID kusalia nchini Sudan mpaka June 2016.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.